VIJANA ndani ya makanisa wameshauriwa kutobweteka kwa kutegemea kuombaomba badala yake wafanya kazi kwa nguvu zote ili kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano ya Dkt John Magufuli.
Kauli hiyo imetolewa na mlezi wa kikundi cha kwaya ya Amani kutoka kanisa la Anglikan Chibwe Parish ya Ndundo,Julias Kiwayawaya alipokuwa akizungumza na vijana kwenye tamasha la uimbaji lililofanyika katika kijiji cha Nhg’ong’ona Mkoani hapa.
Alisema pamoja na shughuli ya uimbaji ya kimungu walizokuwanazo pia wanatakiwa kutumia nafasi waliyokuwanayo ya ujana kufanya kazi kwa nguvu zote ili kuunga juhudi zinazofanywa na serikali.
“Nyinyi kama vijana mnalo jukumu kubwa sana la kuhakikisha mnaiunga mkono serikali yetu hii ya awamu ya tano,kwa kufanya kazi huku mkiibua miradi,na huku mkiendelea kumtumikia mungu siku zote za maisha yenu”alisema.
Alisema katika nafasi walizokuwanazo pia wanatakiwa kuunda vikundi vya pamoja vya ujasirimali ili waweze kuomba mikopo itakayofanya kuongeza uchumi kwa upande wao binafsi na hata kwa kanisa.
Alisema wakianzisha vikundi hivyo vya ujasirimali na kuomba mikopo wataweza kufanisha hata na kurekodi nyimbo zao,badala ya kusubiri kuwekewa chombo cha sadaka ili waweze kuchangiwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi hicho cha uimbaji Noel Nzalinze alisema lengo la tamasha ni kuweza kupata kiasi cha shilingi million nne ili ziwawezeshe kufanikisha kwenda kurekodi.
Alisema mpaka wanafikia hatua hiyo ya kufanya tamasha tayari wameweza kuwanazo kiasi cha shilingi milioni moja,na mategemeo yake ni kuona waumini mbalimbali wanajitoa ili kufanikisha malengo hayo.
Katika tamasha hilo kwaya hiyo ya Imani iliweza kufanikiwa kupata jumla ya shilingi milioni 3.1 huku ahadi zikipatikana kiasi cha shilingi laki 5.
No comments
Post a Comment