Na John Banda Dodoma
MAASKOFU Mkoani Dodoma wamewaomba Watanzania
kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Magufuli aendelee
kuisafisha Nchi ambayo iligubikwa na harufu ya ufisadi, rushwa pamoja na
kutokuwajibika kwa watendaji wake.
Kauli hiyo imetolewa jana Mjini hapa na Maaskofu hao
kwa nyakati tofauti katika ibada ya kuzaliwa Yesu Kristo.
Kwa upande wake Askofu Amos Kinyunyu wa Kanisa la KKKT
Dayosisi ya Dodoma aliwataka Watanzania kuzidi kumuombea Rais Magufuli kutokana
na utendaji kazi unaowagusa Watanzania wa hali ya chini.
Alisema wao kama kanisa wataendelea kumuombea ili
aweze kufanya kazi anayoendelea kufanya
sasa hivi kwani hata vitabu vitakatifu vinataka usawa katika uchumi wa kipato
kwa kila mtu.
‘’Tunawaomba Watanzania wazidi kumuombea Rais wetu
kasi aliyonayo aendelee kuwa nayo kwani Mungu anapenda haki katika maisha
pamoja na uchumi uliosawa’’
‘’Wakati mwingine hii kauli ya hapa kazi tu inakuwa
hata sisi inatuogopesha lakini Mungu ataendelea kumlinda na kumwongoza’’alisema
Naye Mchungaji kiongozi wa Kanisa la Tanzania
Assembles of God (CCC)Miuji Dodoma,Samson Mkuyi alisema utawala wa Rais
Magufuli unaonekana kuwa ni jibu la Watanzania wengi pamoja na kanisa.
Mchungaji Mkuyi alisema wanafurahishwa na utendaji
kazi wake hasa kwenye upande wa maadili ikizingatiwa kuwa kanisa linataka
maadili ya kiroho na kimwili.
‘’Tulianza kuyaomba haya miaka mitano sisi kama
kanisa tunamwambia asiogope kwani Mungu yupo pamoja na yeye,sisi tunaendelea kumuombea
ili mungu aendelee kumpa ulinzi’’alisema
Kwa upande wake Askofu la Kanisa la Anglikani Central
Tanganyika Dayosisi ya Kati,Dk Dickson Chilongani aliwataka Watanzania
kumuombea Rais Magufuli pamoja na Baraza lake la Mawaziri ili waweze kuwafanyia kazi Watanzania.
‘’Rais ameonekana kutumbua majipu yaliyokuwa
yamejificha katika hili tutaendelea kumuombea ili aweze kuyayatumbua zaidi,pia
na kuwafanya watendaji wafanye kazi kwa usahihi’’alisema
mwisho
No comments
Post a Comment