Na Peter Mkwavila Dodoma.
JUMUIYA ya kiislamu ya Ahmadiyya Tanzania imetoa
msaada wa kilo 500 za unga,sukari,maharage,na chumvi kwa shule ya sekondari
Mpunguzi iliyopo mkoani Dodoma kutokana na kuathiriwa na mvua ya mafuriko
iliyoambatana na upepo mkali.
Akizungumza wakati akikabidhi msaada huo Sheikh wa
kanda ya kati wa Jumuiya hiyo Bashart Ur Rehman Batt msaada huo umetolewa
kuunga mkono wito wa serikali inayohimiza mashirika,taasisi,na watu binafsi
kutoa misaada kwa jamii yenye uhitaji.
“Jumuiya ya Ahmadiyya ni moja ya sehemu inayojihusisha
na utoaji wa misaada mbalimbali ikiwemo ya kiafya,kielimu na kijamii kwa
kuwafikia watu wenye uhitaji kama wanafunzi hawa wa shule ya Mpunguzi”alisema.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule hiyo Esther
Milang’tone aliomba mashirika na taasisi zingine yakiwemo madhehebu ya dini
kuelekeza misaada katika shule hiyo ambayo imekutwa na maafa ya mafuriko na
kuharibu miundombinu ya shule hiyo.
“Ni kweli
tulipata mafuriko na asilimia kubwa ya miundo mbinu ya shule hiyo iliharibiwa
ikiwemo chakula na vifaa mbalimbali vya wanafunzi vilisombwa na maji”alisema.
Wakizungumza wanafunzi wa shule hiyo kwa niaba ya
wenzao Zipora Elisha na Kelvin Ludovic walisema walikuwa wanashindwa kuingia
madarasani kutokana na ukosefu wa chakula,hivyo kupatikana kwa msaada huo wana
uhakika wa kufanya vizuri kwenye taaluma.
“Tunaishukuru taasisi ya Ahmadiyya kwa kutuwezesha
msaada wa chakula tunapenda kuhakikisha kuwa tutasoma kwa umakini kwa kuwa tatizo
la njaa shuleni hapo litakuwa limepungua”alisema.
Naye mkuu wa wilaya ya Dodoma Dr Jasmini Tisekwa
alisema anaishukuru taasisi hiyo kwa kuunga mkono jitihada za serikali pindi
yanapotokea maafa mbalimbali.
Imeandaliwa na peter mkwavila
Mhariri: Denice J Kazenzele
Januari/27/2016
No comments
Post a Comment