Na John Banda, Chemba
CHAMA cha wafugaji (CCWT) wilayani Chemba mkoani
Dodoma kimelalamikia kitendo cha watumishi wa halmashauri hiyo kuwatoza fedha za
michango mbalimbali ikiwemo mfuko wa
maendeleo ya elimu kwa kutumia stakabadhi feki zinazo changia kupotea kwa
mapato ya serikali.
Wafugaji hao waliyasema hayo juzi wakati wakizungumza
na na Jambo leo wilayani hapa.
Katibu wa chama hicho wilayani hapa Saidi
Nghambi, alisema kuwa watendaji wa vijiji mbalimbali wamekuwa wakiwatoza pesa
za mchango huo wa mfuko wa jimbo kwa kutumia stakabadhi feki tofauti na zile za
halmashauri hali inayosababisha upotevu wa mapato ya ndani.
Nghambi alisema kuwa watendaji wa vijiji wilayani
hapa pamoja na wale wa vitongoji na vijiji wamekuwa wakichangisha michango hiyo
kwa kutumia stakabadhi za madukani ambazo hazina muhuri wala nembo ya halmashauri.
“Tunachangishwa lakini stakabadhi unayopewa ni
ile ya dukani kama zile tunazo pewa na wauzaji wa maduka ya vifaa vya ujenzi au
vyakula”alisema Nghambi.
Aidha alisema kuwa wamekuwa wakilalamika katika
ngazi mbalimbali pamoja na kupeleka ushahidi wa stakabidhi hizo ambazo
zinatumiwa na watendaji hao lakini hakuna hatua zilizo chuliwa hadi hivi sasa.
“Tuliandika barua kwenda kwa waziri mkuu wakati ule
wa serikali ya awamu ya nne, mkuu wa mkoa wa Dodoma akapewa jukumu la
kulishughulikia suala hili lakini hadi hivi sasa hakuna hatua zilizo chukuliwa”alisema
Nghambi.
Alisema kuwa pamoja na kuchangishwa michango hiyo
lakini hakuna sheria iliyopitishwa na vikao vya halmashauri kuwataka kuchangia
mchango huo wa mfuko wa elimu.
“Hiki kinachofanyika ni kile kinachotokana na
sheria za wilaya tuliyotengana nayo ya Kondoa lakini sisi hapa bado hatuna
sheria hiyo ya mfuko wa elimu” alisema Nghambi.
Naye mwenyekiti wa chama hicho cha wafugaji
Salamba Mataji, alisema kuwa hali hiyo imekuwa kero kwao kutokana na
kuchangishwa michango mingi lakini stakabadhi wanazopatiwa ni feki.
“Tulishakwenda hadi kwa mkurugenzi lakini
hakutusikiliza na kutuambia sisi wafugaji wajinga na kutufukuza bila
kutusikiliza”alisema Mataji.
Mataji alisema kuwa hivi sasa wanajipanga
kumwandikia barua Rais Dk, John Magufuli ili aweze kuwasaidia katika kuondokana
na adha hiyo ambayo wameipata kwa kipindi kirefu.
“Wafugaji wa Wilaya hii tumenyanyasika kwa muda
mrefu sana hivyo basi tunataka kwenda kumuona mweshimiwa Rais”alisema Mataji.
Akijibu malalamikoa hayo Mkurugenzi wa halmashauri
hiyo Dk, William Mafwele, alisema kuwa suala la kuwepo kwa sheria ya mfuko huo
wa elimu tayari lilishapitishwa na baraza la madiwani.
“Kama ni suala la sheria ipo ila hilo suala la stakabadhi
feki ambazo watendaji wanazitumia kwa kuwapatia wafugaji hilo ni kosa la jinai na
wafugaji wanatakiwa wakatae kutoa fedha zao kama hakuna stakabadhi
zinazotambulika na halmashauri ”alifafanua Dk Mafwele
Mwandishi:John Banda
Mhariri: Denice J. Kazenzele
January /27/2016
No comments
Post a Comment