LEO timu yetu ya Taifa, Taifa Stars iliyopo kundi G katika michuano ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa Afrika inaumana na Misri katika mchezo utakaochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kundi hilo linaundwa na timu nne huku kukiwa na jumla ya makundi 13 ya timu nne nne ambayo kupitia makundi hayo ndipo yatatoka majina halisi ya timu, ambazo zitacheza fainali za Kombe la Mataifa Afrika mwakani nchini Gabon.
Timu hizo zimekuwa zikicheza michezo ya ndani na nje ya nchi kuanzia Juni 2015 hadi Septemba mwaka huu na kundi hilo lina timu nne, ambazo ni Nigeria, Misri,Tanzania pamoja na Chad, ambayo ilijitoa.
Kujitoa kwa Chad Lakini hata hivyo inaonekana kuwa Machi 27 mwaka huu, Chad ilitangaza kujitoa katika michuano hiyo kutokana na uhaba wa fedha unaoikabili nchi hiyo.
Kutokana na taratibu ni kwamba kwa timu ambayo inajitoa basi ndio hata zile pointi ilizokuwa amezipata zinapokwa. Lakini pia hata ile michezo ambayo timu hiyo ilikuwa imepangwa kucheza nazo inafutwa.
Mchezo huu wa Misri na Taifa Stars unachezwa huku timu ya Nigeria, Super Eagles ikiwa tayari imeshafahamika kuwa imeshindwa kufuzu katika michuano hiyo itakayochezwa Gabon.
Hiyo ni baada ya kufungwa 3-0 na Misri katika mchezo wao huo uliochezwa katika Uwanja wa Borg El Arab uliopo, Alexandria. Pia katika mchezo wa pili, Misri ilitoka sare ya 1-1 katika mchezo uliokuja kuchezwa Kaduna, Nigeria.
Wamisri hao wanakuja kucheza mchezo wao huo wa leo wakiwa na ghadhabu ya ushindi kutokana na kukosa mara tatu ubingwa huo.
Kwa sasa wakiwa wanaongoza kundi lao wakiwa na pointi saba wanaonekana ni dhahiri kuwa wamejipanga vema kwa mchezo wao huo wa leo hasa kutokana na ushindi ilioupata katika michezo iliyopita.
Kufuzu kwa Misri Misri inahitaji sare tu dhidi ya Taifa Stars ili iweze kukata tiketi ya kufuzu kucheza fainali za Gabon 2017.
Stars inatakiwa kucheza ikiwa na tahadhari kubwa ya wachezaji wa Misri, ambao wengi wao wanatoka katika klabu kubwa nchini humo kama Al-Alhy, Zamalek na zingine. Pamoja na Misri kuonekana kufanya vizuri, lakini Taifa Stars inaweza kuifunga Misri endapo tu itagangamala na kucheza kwa ari kubwa.
Endapo Stars itashinda leo, basi itarejesha matumaini ya kufuzu kwa mara ya pili fainali hizo baada ya zile za mwaka 1980 nchini Nigeria ilizocheza kwa mara ya mwisho.
Stars katika mchezo wake wa kwanza ilifungwa na Misri 3-0 mwaka jana wakati ikiwa na kocha wake Mart Nooij na ndicho kilikuwa chanzo za kocha huyo kuondolewa kukinoa kikosi hicho. Huku kwa sasa kikiwa chini ya Charles Mkwasa ambaye ni mzawa na alipewa jukumu la kuinoa timu hiyo kwa sasa anasema kuwa ana imani kuwa anaweza kuwanoa mafarao hao wa Misri.
Ni dhahiri kuwa wachezaji wa Stars wanaweza kucheza wakiwa na nia ya dhati hasa zaidi kwa kuwa wanakuwa wakichezea uwanja wa nyumbani hivyo wana kila sababu ya kushinda. Mkwasa anasema kuwa ushindi ni lazima kwa kuwa wachezaji wake wamekuwa wakitumia muda mwingi zaidi kujituma kimazoezi. Alisema kuwa mchezo huo kazi moja kubwa itakuwa ni ushambuliaji na pia uchezaji unaozingatia nia na kujituma. Anasema kuwa kwa sasa wachezaji wote wapo salama na wanaendelea na uchezaji wa hali na mali wakiwa mazoezini.
Aliongeza kuwa watahakikisha kuwa wanashambulia zaidi ili kufanikisha adhma yao ya ushindi. “Tunatambua nafsi ya mchezo huu kwa timu yetu na taifa zima kwa ujumla na wachezaji hawa wapo katika hali nzuri ya kimchezo na hakuna majeruhi hadi sasa,” alisema kocha huyo. Mchezaji wa timu hiyo anayechezea timu ya Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta anasema kuwa mchezo wa kesho ni ushindi tu.
Anasema kuwa wachezaji wamejipanga vya kutosha na kuwa ushindi ni lazima kwa kuwa hakuna sababu ya kufungwa katika mchezo huo. “Wachezaji wapo poa kabisa kocha naye yupo safi na wachezaji wanahitaji ushindi kitu ambacho leo ni lazima waone tukifanya hivyo,” alisema. Ni vema kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kuunga mkono timu yetu kwa kuwa wanaweza kufanya vema iwapo tukiwahamasisha.
Katika hili ni vema kwa wote kwa pamoja tukaungana kuanzia na mwenye ngoma, kanga, tarumbeta na mengineo yote kujitokeza kwenda kahamasisha.
No comments
Post a Comment