Mwanajeshi aliyenusurika kifo, Roman Valutov. |
Roman Valutov akiwa katika pozi. |
Bado Urusi ipo kwenye hali ya sintofahamu kufuatia ajali mbaya ya ndege, iliyotokea juzi na kusababisha vifo vya watu 91, wakiwemo wanakwaya wa jeshi wa kikosi cha Red Army Alexandrov, waliokuwa wakielekea Latakia nchini Syria, tayari Rais Vladmir Putin wa Urusi, amevitaka vyombo vinavyohusika kufanya kazi yake na kumpelekea ripoti ya kilichosababisha ajali hiyo.
Wakati abiria wote waliokuwa ndani ya ndege hiyo wakipoteza maisha, ipo simulizi ya kusisimua juu ya mwanajeshi ambaye alipaswa kuwa ndani ya ndege hiyo lakini akazuiwa uwanja wa ndege kusafiri baada ya kubainika kwamba hati yake ya kusafiria ilikuwa ime-expire tangu mwezi wa saba.
Ilikuwaje? Akisimulia mkasa huo huku akitokwa na machozi, mwanajeshi huyo, Roman Valutov, 29, alisema:
“Nilikuwa kwenye orodha ya watu waliopaswa kusafiri na bendi yetu kuelekea nchini Syria. Nilishajiandaa kwa kila kitu lakini tukiwa uwanjani hapo, ilipofika zamu yangu kwenda kukaguliwa, dada aliyekuwa kwenye ofisi ya uhamiaji, alinitazama kwa macho ya mshangao.
“Nikamuuliza kulikoni? Akaniambia ananishangaa kupanga mstari pale wakati najua kwamba hati yangu ya kusafiria ilishaisha muda wake tangu Julai, nikamwambia sikuwa najua. Ilibidi niwekwe pembeni na maafisa wa uwanja huo, wakaanza kujadiliana nini cha kufanya.
“Wakati huo wenzangu waliendelea kukaguliwa na hatimaye wakaelekea kwenye ndege. Nilipouliza kuhusu hatma yangu, niliambiwa ‘huendi popote, paspoti yako imeisha muda wake.’ Nilisikitika sana kwa sababu nilipenda kusafiri na wenzangu lakini sikuwa na ujanja.
“Ilibidi nirudi nyumbani kupumzika. Baadaye nikashangaa simu imeanza kuita mfululizo, watu wengi wakawa wananipigia na kuniuliza kama nipo hai, nikawauliza kumetokea nini? Wakaniambiandege imepata ajali na jina langu lilikuwa miongoni mwa watu waliotangazwa kwamba wamekufa kwenye ajali hiyo, nilipata na mshtuko mkubwa sana. Ndugu zangu nao walikuwa kwenye taharuki, ni tukio la ajabu sana, ahsante Mungu kwamba bado naishi.”
Chanzo:Global Publisher
No comments
Post a Comment