Utata umegubika mdahalo wa moja kwa moja ambao unafaa kuwashirikisha
wagombea wenza wa urais nchini Kenya.
Mdahalo huo, ambao utapeperushwa kupitia runinga, umepangiwa kufanyika
leo jioni.
Hata hivyo, baadhi ya wagombea wenza wa urais wametangaza kwamba
hawatashiriki katika mdahalo huo utakaofanyika katika Chuo Kikuu cha Kanisa
Katoliki cha Afrika Mashariki (CUEA).
Miongoni mwa waliojitoa kutoka kwenye mdahalo huo ni mgombea mwenza wa
chama cha Jubilee chake Rais Kenyatta, Naibu Rais William Ruto.
Mgombea mwenza wa muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa),
wake Raila Odinga, Makamu Rais wa zamani Kalonzo Muysoka pia ametangaza kwamba
hapangi kuhudhuria mdahalo huo.
Chama cha Jubilee kilikuwa kimedokeza kwamba kitamtuma mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung'wa, ambaye hana mtu
anayempinga uchaguzini eneo bunge lake, angemuwakilisha Bw Ruto.
Kwa mujibu wa gazeti
la Standard la Kenya, wagombea wenza Eliud Kariara, Emmanuel Nzai, Joseph
Momanyi, Miriam Mutua, Titus N'getuny na Moses Maranga walikuwa wamemwandikia
mwenyektii waandalizi wa mdahalo huo Debates Media Limited Wachira Waruru
kusema hawakuwa wamepokea mawasiliano yoyote kuhusu mpangilio wa mdahalo huo.
Waandalizi
hata hivyo walikuwa wamesema kwamba watawakubali wagombea wenzake pekee na
kwamba mdahalo huo utaendelea kama ilivyopangwa.
Mdahalo
wa wagombea urais umepangiwa kufanyika Jumatatu wiki ijayo.
Bw
Kenyatta pia ametishia kutohudhuria mdahalo huo sawa na Bw Odinga.
Wawili
hao walisema kuwa hawakushirikishwa wakati wa maandalizi ya mdahalo huo, na
hawafurahishwi na mpangilio wake.
Wakati huo huo,Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa Kenya imewatahadharisha wasimamizi wa makundi ya mawasiliano katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp kwamba watachukuliwa hatua makundi yao yakitumiwa kueneza chuki.
Tume hiyo imesema kwamba itakabiliana vilivyo na watu watakaotoa matamshi ya chuki na kikabila nchini humo, wakati huu wa kampeini za uchaguzi mkuu.
Uchaguzi mkuu nchini Kenya utafanyika mnamo tarehe 8 mwezi Agosti.
"Enyi wasimamizi wa makundi ya WhatsApp ambao makundi yenu yanatumiwa kusambaza ujumbe wa chuki, hebu tuwe makini," amesema mwenyekiti wa tume hiyo Francis Kaparo, ambaye zamani alikuwa spika wa bunge la Kenya.
Amesema tume hiyo imeyatambua makundi zaidi ya 21 ya WhatsApp ambayo yanatumiwa kueneza chuki.
Bw Kaparo pia amewaonya wanasiasa ambao watatoa matamshi ya uchochezi, matusi, taarifa za uongo, yanayodhalilisha mtu au watu kingono au ya kukudunisha kikabila.
Bw Kaparo amesema "watakiona cha mtema kuni".
Aidha watumiaji wa simu za rununu pia wameonywa dhidi ya kusambaza ujumbe ambao unaweza kusababisha taharuki au vita vya kikabila.
Polisi wameshauriwa kuwakamata watu wanaokiuka tahadhari hiyo iliyotolewa huku kampuni za rununu na mitandao ya kijamii zikiombwa kuondoa ujumbe ambao wanaona unaweza kuingiza taifa katika lindi la vita na umwagikaji wa damu.
Mkuu wa jeshi la polisi nchini Kenya Joseph Boinnet mapema leo Jumatatu, amesema kuwa kikosi chake "kitatumia nguvu zaidi" dhidi ya watakaosababisha vurugu.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2007/08, zaidi ya watu 1,133 waliuawa na zaidi ya watu nusu milioni wakaachwa bila makao baada ya ghasia kuzuka.
No comments
Post a Comment