Abiria 12 wamefariki dunia leo mkoani Iringa na
wengine 28 wamejeruhiwa vibaya baada ya basi la abiria la kampuni ya
New Force kugongana na lori maeneo ya Igeme, Kilolo mchana wa leo.
Kufuatia ajali hiyo watu wasiopungua 12 wamefariki dunia papo hapo huku makumi ya wengine wakijeruhiwa. Taarifa zaidi zinasema, majeruhi 28 hali zao ni mbaya sana.
Jeshi la Polisi mkoani Iringa limethibisha kutokea ajali hiyo na kuongeza kuwa majeruhi wamewahishwa hospitali ya wilaya ya Kilolo huku wengine waliokuwa taabani wamekimbizwa hospitali ya mkoa wa Iringa kwa ajili ya matibabu.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Iringa, madereva wa basi na lori ni miongoni mwa watu waliojeruhiwa katika ajali hiyo na uchunguzi unaendelea.
Tanzania imekuwa ikishuhudia ajali za mara kwa mara za barabarani ambapo makumi ya watu wamekuwa wakipoteza maisha yao na wengine kujeruhiwa au hata kupata vilema vya maisha. Uchunguzi uliofanywa unaonesha kuwa, uzembe wa madereva na mwendo wa kasi ndizo sababu kuu mbili zinazosababisha mlolongo wa ajali za barabarani nchini Tanzania.
No comments
Post a Comment