Serikali
mkoani Singida, imewataka wananchi kuhakikisha wanatumia vyema fursa ya
uwepo wa huduma zinazotolewa na madaktari bingwa, ili waweze kupatiwa ufumbuzi
wa matatizo ya maradhi mbalimbali yakiwemo ya moyo na koo.
Wito
huo umetolewa na mkuu wa mkoa wa Singida, Dk. Parseko Kone, wakati akizungumza
kwenye uzinduzi wa huduma zitakazotolewa kwa kipindi cha wiki nzima na
madaktari bingwa katika hospitali ya mkoa kwa kusema mpango wa mfuko wa
Taifa wa bima ya afya (NHIF) kuleta madaktari bingwa watano wa magonjwa
mbalimbali mkoani hapa, utawapa nafasi wananchi wengi kupata huduma na
ushauri ambao hulazimika kuutafuta nje ya mkoa,hata kuvuka mipaka na kwenda
nchi jirani.
Akifafanua
zaidi, Dk.Kone amesema kwa miaka mingi wakazi wa mkoa huu wamekuwa wakiingia
gharama kubwa kusaka huduma za madaktari bingwa,hivyo uwepo wa madaktari hao
hivi sasa,utawapunguzia gharama kwa wale watakaobahatika kuonana nao.
Aidha
mkuu huyo wa mkoa ameupongeza kwa dhati uongozi wa NHIF, kwa kubuni mpango huo
ambao una umuhimu na manufaa makubwa, kwa wakazi wa mkoa wa Singida.
Awali, Kaimu mkurugenzi mkuu NHIF, Michael Mhando,ameeleza lengo la mpango wa kupeleka madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali mikoani, ni kuwapunguzia wananchi adha ya upatikanaji wa madaktari bingwa mpango ambao unatoa huduma kwa wananchi bila kujali kipato chake, ambapo hadi sasa umefikia mikoa 13 ukiwemo mkoa wa Singida, zoezi ambalo ambalo litaendelea katika mikoa yote nchini.
Mbali kutoa huduma ya za kiafya pia wametoa msaada wa vifaa vya tiba na mashuka 300, vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni tano, huku akiahidi mfuko huo kuendelea kuiunga mkono serikali ya mkoa kwa kuboresha sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Rufaa.
Wakati huo huo Mchungaji wa kanisa la kilokole la Pentekoste kijiji cha Itaja
tarafa ya Mgori wilaya ya Singida David Mtipa (59) na mke wake Maria Philipo
(45),wamepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi mjini hapa, kwa
kosa la kushindwa kumpatia huduma muhimu mtoto wao, na kumsababishia madhara ya
kudumu kiafya .
Wana ndoa hao wanatuhumiwa kushindwa kumpatia huduma muhimu mtoto
wao Timotheo (30) kwa kipindi cha miaka 12 mfululizo.
Mapema mwendesha mashitaka mwanasheria wa serikali,Patrisha
Mkina,alidai mbele ya hakimu mwandamizi wa mahakama hiyo,Faisal Kahamba,kuwa
kati ya mwaka 2003 na 2015,kwa makusudi mchungaji David akishirikiana na mke
wake Maria,walishindwa kumpatia mtoto wao Timotheo huduma muhimu za kibinadamu.
Aidha ameongeza kuwa wana ndoa hao walitenda kosa hilo,huku
wakijua wazi kuwa kitendo hicho ni kinyume na sheria namba 229 kanuni ya adhabu
ujazo wa pili wa sheria kama ilivyofanyiwa marekebesho mwaka 2002.
Akifafanua,Mkina amesema kwa kipindi cha miaka 12,washitakiwa kwa
pamoja walimnyima Timotheo,makazi,chakula,nguo,matibabu na uhuru wake wa
kikatiba,kitendo ambacho kimechangia apate madhara ya kudumu ya afya yake.
Washitakiwa kila mmoja kwa wakati wake wamekana shitaka hilo,na
kesi hiyo itatajwa tena desemba 28 mwaka huu.
Aidha,washitakiwa wapo rumande ya magereza baada ya kushindwa
kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni,kuwa na wadhamini wawili ambao watasaini
dhamana ya shilingi milioni moja kila mmoja.
Wakati huo huo,Joshua (25) mdogo wake na Timotheo,amesema baada ya
wazazi wake kupelekwa rumande,ameshindwa kumpeleka kaka yake nyumbani licha ya
kuruhusiwa kutoka wodi namba nne katika hospitali ya mkoa mjini hapa.
Mwandishi: Ramadhan Rajab
kutoka Singida
18/12/2015
mhariri: Denis Kazenzele
No comments
Post a Comment