Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) linamaliza siku ya 15 likiwa
halina kiongozi baada ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, Dk Ramadhan Dau
kuteuliwa kuwa balozi na kuacha mara moja shughuli za kila siku za
taasisi hiyo kubwa, hali iliyofanya shughuli zake kudorora.
Rais
John Magufuli alimteua Dk Dau kuwa balozi Februari 15, sambamba na
makada wengine wawili wa CCM, Dk Asha Rose Migiro na Mathias Chikawe,
akisema vituo vyao vya kazi vitajulikana baada ya taratibu za
kidiplomasia kukamilika.
Tangu wakati huo, NSSF imekuwa
ikijiendesha bila ya kiongozi mkuu na habari kutoka ndani ya shirika
hilo zinasema kuwa shughuli za shirika hilo kubwa kuliko yote
yanayojihusisha na hifadhi ya jamii nchini, haziendi kutokana na
kutokuwapo na mtu aliyepewa jukumu la kukaimu nafasi hiyo.
Miongoni
mwa mambo hayo ni ufunguzi wa Daraja la Kigamboni jijini Dar es Salaam
ambalo lilitakiwa lianze rasmi kutumika Machi Mosi, ununuzi wa magari ya
ofisi za mikoa, mkutano wa wanachama wa mwaka pamoja na wiki ya NSSF
ambayo hujumuisha mambo mbalimbali, kama shughuli za kijamii, maonyesho
ya huduma za NSSF na michezo.
Juhudi za kumpata Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama, anayehusika na mifuko ya hifadhi
ya jamii hazikufanikiwa. Pia, Katibu Mkuu Kiongozi Ombeni Sefue, ambaye
amekuwa akitoa taarifa za uteuzi unaofanywa na Rais, hakupatikana jana.
Wiki iliyopita, Balozi Sefue alisema maswali kuhusu uteuzi wa
kaimu yaelekezwe kwa Mhagama, ambaye alieleza wakati huo kuwa utaratibu
wa kuimpata kaimu unaendelea.
Kwa mujibu wa ripoti ya fedha ya mwaka
2011, shirika hilo lilikuwa na wanachama 501,218, kati yao wafanyakazi
waliosajiliwa waliongezeka kutoka 17,666 hadi 18,779, sawa na ongezeko
la asilimia 6, huku michango ikiongezeka kutoka Sh300.08 bilioni hadi
Sh356.5 bilioni kwa mwaka, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18.8.
Kwa
mujibu wa muundo wa uongozi wa NSSF, Mkurugenzi Mkuu ndiye kiongozi
mkuu wa shirika akiwa na wakurugenzi wanane chini yake.
Wakurugenzi hao
wanahusika na uendeshaji (DO); utawala na rasilimali watu (DHRA);
mipango, uwekezaji na miradi (DPIP); fedha (DF); teknohama (DIT);
ukaguzi wa ndani (DIA); uthibiti na usalama wa mali (DARM) na huduma za
kisheria (DLS).
No comments
Post a Comment