NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amefanya ziara katika halmashauri mpya ya Itigi na Manyoni huku akibaini uwepo wa changamoto mbalimbali hususan upungufu wa dawa katika Kituo cha Afya Itigi na Hospitali ya wilaya ya Manyoni mkoani Singida.
Akizungumza katika ziara hiyo, Jafo amesema mara baada ya kutembelea Halmashauri hizo amebaini changamoto za dawa katika kituo cha afya Itigi pamoja na vifaa katika chumba cha mama huku akisema zipo changamoto ambazo zinazotakiwa kutatuliwa ndani ya halmashauri hiyo.
Jafo akizungumza kuhusu suala la upatikanaji wa dawa, amesema tatizo hilo linaonekana ni kikwazo kutokana na watendaji kushindwa kutumia fedha za dharura wanazopewa na serikali kununulia dawa na vifaa tiba.
“Naziagiza Halmashauri hizi kuhakikisha zinaweka kipaumbele uboreshaji wa vituo vya afya kwa kununua dawa nyingi na vifaa vingine tofauti na kusubiri zinazotoka Bohari ya Madawa (MSD),”amesema Naibu Waziri huyo
Amewaagiza watendaji wa idara mbalimbali kuhakikisha wanashirikiana na mkurugenzi wa Itigi ili kutimiza wajibu wao na kuifanya halmashauri hiyo kuwa bora na kuwaonya kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
“Kila mtumishi ahakikishe anajali muda wa kazi na kuacha tabia ya kutoenda kwa ratiba ya kazi, watumishi wa Tamisemi wanatakiwa kujiamini katika kazi zao na kuacha uoga ama kufanya kazi hadi pale wanapofuatiliwa hasa kwenye miradi mbalimbali,”amesema
Kadhalika, Naibu Waziri huyo amewataka wahasibu kuacha tabia ya kuabudiwa kutokana na kuamua kuidhinisha fedha hadi pale watakapojisikia na kusababisha miradi mingi kukwama na mingine kufa.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa hospitali ya wilaya ya Manyoni, Dk. Francis Mwanisa, amesema hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu wa dawa licha ya kupokea wagonjwa kutoka sehemu mbalimbali nje ya wilaya hiyo.
No comments
Post a Comment