Korea Kaskazini imesema Rais Donald Trump wa Marekani na serikali yake "wanabembeleza vitokee vita vya nyuklia" huku Washington na muitifaki wake katika Peninsula ya Korea, yaani Korea Kusini zikijiandaa kufanya manuva makubwa ya kijeshi ya angani.
Taarifa hiyo ya wizara ya mambo ya nje ya Korea Kaskazini imetolewa katika hali ambayo Marekani na Korea Kusini zinajiandaa kwa mazoezi ya kijeshi yaliyopewa jina la Vigilant Ace yaliyopangwa kuanza Jumatatu ya kesho. Askari wapatao 12,000 wa jeshi la Marekani na ndege za kivita 230 wanatazamiwa kushiriki kwenye manuva hayo.
Hayo yanajiri huku kauli za vitisho zinazotolewa na Marekani dhidi ya Korea Kaskazini zikikabiliwa na ukosoaji mkali.
Baada ya Korea Kaskazini kulifanyia majaribio kombora lake la balistiki la masafa marefu zaidi, mapema wiki hii balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley aliionya serikali ya Pyongyang kuwa nchi hiyo inaweza "kuangamizwa kikamilifu" endapo vita vitatokea kati yake na Washington.
Hata hivyo matamshi hayo ya Haley yalikosolewa vikali na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov, ambaye siku ya Ijumaa alisema: "kama kuna mtu aliyedhamiria kikweli kutumia nguvu, kama alivyoeleza mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ili kuiangamiza Korea Kaskazini.. nadhani atakuwa anachezea moto na kufanya kosa kubwa".
Korea Kaskazini inakabiliwa na vikwazo mbalimbali vya kimataifa vya kuishinikiza isimamishe mipango yake ya nyuklia na makombora. Hata hivyo imepuuza mashinikizo yote yanayotolewa dhidi yake huku ikiapa kuwa haitoachana na mipango yake ya nyuklia na makombora kutokana na vitisho na uadui wa Marekani dhidi ya nchi hiyo.
No comments
Post a Comment